Thursday, December 12, 2013

HARAMBEE STARS

The Stars are shining bright,

Held up by the spirit of Harambee,

In the darkness of the night,

Fiftieth birthday present you’ll be,

Giving Kenya it’s long lost light,

You stung Sudan like a bee,

Marking the opponents tight,

Two-zero let it be,

The Challenge Cup is your right,

Hail the Stars of Harambee,

Today they have shown their might.

©Samuel Mwenda 2013

Sunday, April 8, 2012

NAIMBA

Naimba mimi siibi, wanoiba hawaimbi,

Natamba nami sishibi, wanoshiba hawatambi,

Napamba mimi shababi,  baba hawabebi tambi,

Naamba sina hababi, Habiba ana vitimbi.Nawaka mimi sioki, wanooka sio sisi,

Nasaka mimi sichoki, wanochoka si wasasi,

Nataka mimi simaki, wanomaka si asasi,

Nashika nami sidaki, wanodaka huakisi.Naita  mimi sisiti, wanosita wameketi,

Nakita mimi sikiti, wasokita ni maiti,

Napita mimi siwati, wanowata wenyeviti,

Nakata mimi sifwati, wanofwata mapingiti.Nikilemewa si kitu, wasolemewa si watu,

Nikiishiwa na kitu, wasoishiwa majitu,

Nikipatiwa si kutu, wasopatiwa vijitu,

Nikipishiwa na mtu, wasopishwa ni msitu.Naomba mimi Yarabi, wanoiba sakubimbi,

Nachimba mimi sizibi, wanoyaziba mafumbi,

Nabamba mimi si bibi, wanoshiba kumbikumbi,

Nakumba mimi sibebi, wanaobeba vimbimbi.Naona mimi moyoni, kiona una maoni,

Nabana mimi sineni, kinena unafitini,

Nasana mimi mbioni, kituna una milioni,

Narina mimi zingani, kijana una uneni?© Tabu Bin Tabu 2012

Friday, April 6, 2012

AT LAST

I have to feast,

I killed the beast,

At least it can't last,

All is dust,

It is the last,

All in my past,

I have to trust,

Let it rest,

I hope for the best,

Can't afford the least

Lest crust will bust

In everlasting  lust.

© TABU BIN TABU

Saturday, February 11, 2012

MADODO YANA WADUDU

Madodo usiyaone, yaning’inia mtini,

Yaonekana manene, yangejaa kiganjani,

Yakakutoka matone, ya mate toka kinywani,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, yamepangwa sakafuni,

Kwenye mafungu manene, yauzwa huko sokoni,

Unayafinya uone, yameiva vidoleni,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, yameiva kwelikweli,

Yakawa rangi nyingine, nyekundu kama kimuli,

Yatakuchoma pengine, kiyatua kwenye mwili,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, yakiwa kwenye gunia,

Maumbo yake uone, ndani yanafinyania,

Ukayatoa unene, wataka kuyapania,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, yamejaa kwenye shamba,

Yamepakwa manemane, rangiye yamejipamba,

Yakinenepa yatune, chunga usifanywe kimba,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, yaning’inizwa kwa kamba,

Ukahesabu manne, mazuri ukayabamba,

Kumbe yanayo manune, yenye meno kama mamba,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, wengine washerekea,

Usende mkazozane, wao kuwapokonyea,

Akuchukie wanune, kumbe umejichongea,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, machoni yatamanika,

Yatakulipa senene, upate kuhuzunika,

Yatakutia unane, hakika tasononeka,

 Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, maji yake kuyaminya,

Ukachukua mashine, sharubati kuifanya,

Ukayanywa na matone, kwa maganda kuyamenya,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.Madodo usiyaone, ukadhani ni matamu,

Kwa tamaa uyachane, kadhani ni ya msimu,

Kama nazi uyakune, usijue yana sumu,

Madodo yana wadudu, jihadhari mtamani.© Tabu Bin Tabu

    24-10-2011

Sunday, January 1, 2012

KUPANDA USIPOPENDA

Ndugu yangu tahadhari, nakwambia waziwazi,

Usijawe na kiburi, ukachukua vya wizi,

Ukijihisi subiri, utafute lahazizi,

Kupanda usipopenda, si kupanda ni kutupa.Usijitie mwapuza, kaimba kazi ni kazi,

Tamaa zako punguza, kwanza upate ujuzi,

Ng’ang’ana takuumiza, roho kipenda maizi,

Kupanda usipopenda, si kupanda ni kutupa.Mapenzi ni njia mbili, upende nawe upendwe,

Mapenzi ya mbwa kali, yasiyopenda yashindwe,

Mapenzi ni ya kibali, asiyependa alindwe,

Kupanda usipopenda, si kupanda ni kutupa.Kung’ang’ania kukutu, kijuwa hautapendwa,

Kupigana kwa mtutu, kigundua umeshindwa,

Kukosa roho ya utu, kwa lazima unapindwa,

Kupanda usipopenda, si kupanda ni kutupa.Kioa asokupenda, si kuoa ni kuzoa,

Kifwata alekuwinda, sidhani amekuoa,

Kidhani atakupenda, ni Mungu takuokoa,

Kupanda usipopenda, si kupanda ni kutupa.Kichapo sio ungwana, hufurahi uchunguni,

Utajiri siyo zana, ukatumia kuwini,

Usuhuba si laana, ukatesa maskini,

Kupanda usipopenda, si kupanda ni kutupa.Rafiki ni wa kulinda, mawi yasije karibu,

Adui ni wa kushinda, kanunua kwa taabu,

Ukaishi kumponda, kwani huna mahabubu,

Kupanda usipopenda, si kupanda ni kutupa.© Samuel Mwenda

Ustadh Tabu Bin Tabu

Karama Antuamuo, Laare.

28-8-2011

Sunday, December 25, 2011

TUNAKUAGA KWAHERI


Mwenda ninaimba wimbo, mamangu kumuimbia,

Japo tumeona mambo, Mungu hatatukimbia,

Nami sitapiga kumbo, uliko nakuambia,


Mama Monika Kinoti, Tunakuaga kwaheri.
Tulikupenda we mama, naye Mungu akatenda,

Kakupa maisha mema, na tena akakulinda,

Japo meenda mapema, ni Mungu akakupenda,


Mungu muweke pasafi, pa watakatifu wako.
Litupeleka shuleni, nasema ubarikiwe,


Tuinuke maishani, kazini tufanikiwe,

Tusikae ujingani, mambo mengi tuelewe,


Asante sana mametu, fahamu tunakupenda.Ulifanya kazi yako, kwa bidii na makini,

Ukayaandaa meko, tukakula kwa amani,


Japo nina sikitiko, nakutungia mizani,


Mama Monika Kinoti, tunakuaga kwaheri. 
TABU BIN TABU
25-12-2011

Friday, December 16, 2011

TUNYUNYIZIE MASHAMBA

Mvua ikipungua, wakulima waumia,

Mimea inaungua, mazao kuangamia,

Hupati cha kuangua, maafa yametimia,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.Miale ile ya jua, inachoma kwa hasira,

Pasipo kunyesha mvua, itatokea hasara,

Sipochukua hatua, kuokoa kwa dharura,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.Sipokuwa nayo maji, ya kunyunyiza shambani,

Sambaza kwenye vijiji, tabaki kuwa jangwani,

Watu takosa mtaji, watabaki masikini,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.Yatengeneze mabwawa, makubwa yenye kujaa,

Tuyakamue maziwa, tusikumbwe nayo njaa,

Maji yake maridhawa, yatufanye mashujaa,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.Tuinunue mitambo, tupige maji mitoni,

Tuchimbe kwa mitaimbo, mitaro hadi shambani,

Tuziimbe zetu nyimbo, za umoja maishani,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.Ya bahari tutumie, tusijali chumvi yake,

Ya vijito tuchumie, tusijali wingi wake,

Ya maziwa tuvamie, tuchimbe mkondo wake,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.Tusitulie jangwani, kungojea kifo chetu,

Tuingilie shambani, tusitumie mitutu,

Kuibia majirani, tukiwapiga kitutu,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.Sipande mimea ile, yataka maji kwa wingi,

Tupande nayo mawele, yatoe mazao mengi,

Tupande mahindi tele, mihogo na wimbi mwingi,

Sitegemee mvua, tunyunyizie mashamba.© Tabu Bin Tabu

    15/11/2011